Tuesday, January 10, 2012

Wanafunzi waliofutiwa matokeo ya Darasa la Saba kurudia mitihani

Mwalimu wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Bungo iliyopo Manispaa ya Morogoro, Asinath Mshana akimwelekeza namna ya kuumba herufi mwanafunzi wa darasa la kwanza, Nesto Robert , shuleni hapo jana baada ya Shule za Msingi nchini kufunguliwa. 


SERIKALI imeamua kwamba watahiniwa 9,629 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika mwaka jana baada ya kugundulika kufanya udanganyifu, warudie mtihani huo Septemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema kiwango cha wanafunzi waliofutiwa matokeo ni kikubwa na hiyo ndiyo sababu pekee iliyoisukuma Serikali kuwapa nafasi ya kurudia mtihani huo.  

Hata hivyo, alisema uamuzi huo unawahusu wanafunzi wale tu waliogundulika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida na kwamba uamuzi huo hautawagusa wanafunzi 107 ambao walifutiwa matokeo yao baada ya kukutwa na majibu.

“Suala hili la majibu kufanana linaonekana limechangiwa zaidi na walimu… lakini pia wazazi wametoa maoni yao na Serikali imeona iwape nafasi nyingine ya kurudia mtihani huu.” 

 Alisema halmashauri kwa kushirikiana na shule zinatakiwa kuandaa utaratibu utakaowawezesha watahiniwa hao kujiandaa kimasomo  mpaka watakapofanya mtihani huo, huku akiagiza wanafunzi hao kujisajili Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kabla ya 30 Januari, mwaka huu.  Alisema kwa shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi waliofutiwa matokeo,  zinaweza kuwaruhusu kuhudhuria darasani pamoja na wanafunzi wa darasa la saba wa mwaka huu, huku zenye idadi kubwa ya wanafunzi akiziagiza kuandaa utaratibu wa kutoa masomo nyakati za jioni.  

Mulugo alisema watahiniwa hao watafanya mtihani huo sambamba na wenzao wa mwaka huu.  Desemba 14, mwaka jana, Serikali ilitangaza matokeo ya darasa la saba ambayo kati ya wanafunzi 983,545 waliofanya mtihani huo, 567,767 sawa na asilimia 58.28 walifaulu, huku ikifuta matokeo ya watahiniwa 9,736. 

Miongoni mwa waliofutiwa matokeo hayo, wanafunzi 94 walikamatwa na karatasi za majibu, wanne walibainika kuandikiwa majibu, tisa walibainika kukariri darasa kinyume na utaratibu na 9,629 walibainika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida.  

Yaunda tume  Waziri huyo alisema Serikali imeunda tume chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), kuchunguza chanzo cha udanganyifu  na  kutoa mapendekezo ya kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika mitihani.  
Alisema taarifa ya uchunguzi wa tume hiyo itatolewa mwishoni mwa Aprili mwaka huu, huku akisema hatua kadhaa zinaendelea kuchukuliwa na mamlaka mbalimbali kwa wahusika.  “Watendaji au taasisi zitakazobainika kuhusika kwa namna yoyote katika udanganyifu zitachukuliwa hatua,” alisema na kuiomba jamii hususan wazazi kujiepusha na udanganyifu kwa kuwalea watoto katika misingi ya maadili, kujiamini na kujitegemea katika maisha.  

Ada shule binafsi  Akizungumzia viwango vikubwa vya ada vinavyotozwa  katika shule binafsi, Waziri Mulugo alisema suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali ikiwa ni pamoja na kupitia kwa undani mfumo mzima wa ulipaji ada ili iweze kutoa uamuzi wa haki kwa pande zote.  

“Kuna shule za dini, binafsi na za jumuiya, zote zinatoza ada kulingana na gharama za ufundishaji. Zipo ambazo hufanya mafunzo kwa njia ya vitendo nje ya nchi… hii ni gharama pia ndiyo maana tunasema kuwa tunahitaji muda zaidi kulishughulikia hili,” alisema.  

Mitalaa  Waziri Mulugo amezionya shule zinazofundisha kwa kutumia mitalaa ya nchi nyingine. Alisema kama kuna haja ya kufanya hivyo, zinatakiwa kuwa na kibali cha Serikali.  

“Kuna shule moja ilikuwa Mwenge, niliifungia kwa kuwa ilikuwa ikifundisha wanafunzi kwa mtalaa wa nchi ya Kongo (DRC). Sasa kuna tetesi kuwa wamehamia eneo la Ubungo na wanaendelea kufundisha, nitakwenda mwenyewe kuhakikisha na kama ni kweli, wahusika watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola,” alisema.  

No comments:

Post a Comment