Tuesday, January 10, 2012

DIAMOND ATESWA JELA



MWANAMUZIKI wa kizazi kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond’, inadaiwa aliteswa mahabusu kwenye Kituo cha Polisi Kati, mkoani hapa.
Madai yanasema kuwa kutokana na ‘msoto’ aliopewa na mahabusu wenzake, Diamond alishindwa kulala na muda mwingi aliutumia akilia.
Chanzo chetu kimepasha kuwa mahabusu wenzake walimbana Diamond na kumng’ang’ania awaimbie nyimbo zake zote, kitu ambacho kilimpa unyonge mwanamuziki huyo.
“Alitaka kukataa lakini kama unavyofahamu, mahabusu wengine ni wababe sana, kwa hiyo walimlazimisha mpaka akaimba, aliimba nyimbo zote lakini wakataka awaburudishe usiku mzima,” kilisema chanzo chetu ambacho ni mmoja wa maafande wa kituo hicho.
Afande huyo, aliyeomba hifadhi ya jina lake aliongeza: “Wakati anaimba wale mahabusu walishangilia ingawa kuna wengine walimhurumia kwa sababu kwanza hakuwa katika ‘mudi’ ya kuimba, pili alichoka kabisa. Fikiria mtu unaimba kwa kulazimishwa, kwa kweli alilia kama mtoto.
“Alijitahidi kuwaomba wale mahabusu wamhurumie kwa sababu amechoka lakini hawakumuelewa. Walizidi kumbana awaimbie. Wakati mwingine walimtajia mpaka nyimbo ambazo siyo zake aimbe. Yaani mikogo na mapozi yake, vyote vilikwisha. 
“Mahabusu na jela siyo pazuri, kule japo wapo wastaarabu lakini wengi wao ni watu wa ovyo na wameshakata tamaa ya maisha. Mara nyingi hao ndiyo wasumbufu na aina hiyo ndiyo waliomtesa Diamond kwa kumlazimisha awaimbie.”
Diamond alipotafutwa juzi ili azungumzie hali hiyo aliyokutana nayo mahabusu Iringa, alidai yupo kwenye kelele.
Hata baada ya kusomewa shauri zima, bado alikataa kutoa jibu kwa sababu yupo sehemu yenye vurugu.
Mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni, Diamond hakupiga simu kufafanua ‘ishu’ hiyo kama alivyoahidi kuwa angemtafuta mwandishi wetu baada ya kupata sehemu iliyotulia.

No comments:

Post a Comment