Tuesday, January 10, 2012

SKENDO YA KADINALI PENGO KUUZA 'UNGA' JIPU PWAA



MKUU wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Madawa ya Kulevya Nchini (Anti Drugs Unit), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa amepasua jipu pwaa kuhusu tuhuma kwamba Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama  Polycarp Kadinali Pengo amekuwa akihusishwa na skendo ya kuuza ‘unga’.
Kamanda Nzowa alifunguka mwishoni mwa wiki iliyopita alipohojiana na mwandishi wetu kwa kusema kuwa katika sheria na kanuni zao za kazi, mtuhumiwa au mtu anayepeleka taarifa kwao kuhusiana na madawa ya kulevya majina yao huwa hayavuji.
“Niseme tu kwamba mtu yeyote ashirikiane na jeshi la polisi kama kuna mtu anafanya biashara hiyo haramu atueleze, taarifa hazivuji na hazitavuja, hiyo ni moja ya kanuni zetu,” alisema Nzowa.
Aliongeza kuwa kutokana na kufuata kanuni hiyo, mwaka jana (2011), vita dhidi ya madawa ya kulevya ilipata mafanikio kwa kukamata kg 264 ukilinganisha na kg 90 za mwaka 2010. 
Bila kutaja jina la mtu, Kamanda Nzowa alisema, kama kuna anayewafahamu wafanyabiashara hiyo haramu, wawe wakubwa au wadogo, wapeleke taarifa zao  na vielelezo ofisini kwake ili watu hao wakamatwe mara moja.
“Nikiri tu kwamba mapambano ni makali na wale tuliowakamata wamepata hasara kubwa. Tumeokoa vijana wetu na wa nje ya nchi, hivi sasa tunatupia macho baharini, bandarini, kwenye viwanja vya ndege, mipakani na kadhalika, nawatahadharisha wanaofanya shughuli hiyo waache maana hawawezi kusalimika,” alionya Nzowa. 

KAULI YA PENGO
Hivi karibuni Kadinali Pengo aliwaeleza vijana wa kanisa analoliongoza aliokutana nao jijini Dar es Salaam kuwa amekuwa akitajwa kuhusika na biashara hiyo haramu ili kunyamazishwa asiharibu maslahi ya genge la wafanyabiashara ya madawa ya kulevya.
Katika hali iliyowashangaza wengi, Kadinali Pengo aliwaeleza vijana hao katika misa maalumu ya ufukweni inayowakutanisha kila mwaka jijini Dar es Salaam kwamba kumekuwa na kundi la watu wanaoamini anaharibu mwenendo wa mipango yao katika biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya.
Kutokana na hali hiyo, Kadinali Pengo aliwaonya vijana kutoendelea kutumika kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakitumika kwa muda mrefu katika biashara hiyo haramu. 
Hata hivyo, kiongozi huyo hakuwataja kwa majina wahusika wa genge hilo ambalo amedai lina mipango ya kumziba mdomo kwa kumzushia kesi hiyo.
Akifafanua zaidi, Pengo alisema, mbinu wanayotumia ya kutaka kumnyamazisha ni pamoja na kutaja jina lake katika orodha ya wafanyabiashara ya mdawa ya kulevya, kitu ambacho amesisitiza hakitamnyamazisha kufichua ukweli kuhusu biashara hiyo haramu.
Aliwataka vijana kutokubali kutumika kwa manufaa ya baadhi ya watu hao wachache ambao kwa sasa wameonesha mwenendo wa kuchukizwa na watu wanaowakosoa, akasema: “Ninyi vijana msikubali kutishwa.”
 Aliweka bayana kuwa watenda maovu wakiwamo wanaouza madawa ya kulevya wako radhi kuwatumia vijana kufanikisha malengo yao, huku wakiwa tayari kuwatishia viongozi wa dini wanapojaribu kukemea uovu wao huo.
Aliwahimiza vijana kupingana na magenge ya  wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya japokuwa hakuwataja na akaongeza:  “Mnao uwezo wa kuwa askari na kupigana nao, silaha yenu si bunduki bali ni ukweli.”
Kauli hiyo ya Kadinali Pengo imekuja miezi kadhaa baada ya kuwapo kwa malumbano kati ya baadhi ya viongozi wa dini na serikali kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete.
JK aliwaambia viongozi wa dini kusaidia vita dhidi ya madawa ya kulevya na kuwataka wale miongoni mwao ambao wanajihusisha nayo kuacha mara moja.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi, aliwahi kumkaribisha Nzowa na timu yake bungeni ambako waliwaonesha wabunge picha za video za baadhi ya wahusika wa madawa ya kulevya, wakiwamo baadhi ya viongozi wa dini.

WANANCHI WAMKOSOA PENGO
Baadhi ya wananchi akiwemo Charles Kiluwa, mkazi wa Masaki Dar es Salaam, walisema kuwa Pengo hakupaswa kusema aliyoyasema kutokana na wadhifa wake katika jamii.
“Mimi nilishtuka sana niliposikia maneno ya Kadinali Pengo, hakupaswa kusema aliyoyasema. Kama kuna mtu anasema yeye yumo angempuuza tu kwa sababu polisi sio wajinga, angekuwemo angehojiwa, aendelee kuwaelimisha vijana kuachana na maovu likiwemo hilo la madawa ya kulevya,” alisema Kiluwa.
Naye Fidea Kichea mkazi wa Oysterbay, Dar, alisema alipata mshituko aliposikia kiongozi huyo wa dini akisema kuna watu wanamtaja kuhusika  na madawa ya kulevya, “Angepuuza tu na kama anawajua angewaambia polisi , mbona waumini wake wanamuelewa kwamba ni mtu safi,” alisema Fidea.

No comments:

Post a Comment