Tuesday, January 10, 2012

Mh Magufuli atangaza neema Kigamboni


SERIKALI jana ilitiliana saini na Kampuni ya China Railways Construction Engineers Group kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni mwezi huu.

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kampuni hiyo kwa kushirikiana na Kampuni ya China Major Bridge, ilishinda zabuni ya kujenga daraja hilo katika kipindi cha miaka mitatu, baada ya Kampuni ya Arab Consulting Engineers kumaliza kazi ya upembuzi yakinifu.

Dk Magufuli alisema daraja hilo la Kigamboni linatarajiwa kugharimu Sh214.6 bilioni, fedha ambazo Serikali itachangia asilimia 40 na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), asilimia 60.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kutia msaini mkataba huo, Dk Magufuli alisema lengo la Serikali kujenga Daraja la Kigamboni ambalo ujenzi wake unaanza mwezi huu ni kuleta maendeleo na kuinua uchumi hivyo kuwataka wananchi kushirikiana nayo ili kuhakikisha kuwa azma hiyo inatekelezwa kwa vitendo na si kuleta maneno.

Alisema NSSF ilitangaza zabuni ya ujenzi wa daraja hilo na kampuni 15 zilijitokeza, saba kati ya hizo ndizo zilizoingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Daraja hilo litahusisha ujenzi wa mita 680, njia sita za lami kwa umbali wa kilomita 1.0 kwa upande wa Kurasini na njia sita za lami kwa umbali wa kilomita 1.5 upande wa Kigamboni.

“Wananachi wa Kigamboni na maeneo mbalimbali wataweza kutumia daraja hilo kwa ajili ya kurahisisha shughuli za maendeleo. Tunapaswa tushirikiane ili kuhakikisha kuwa daraja hilo linakamilika kwa muda uliopangwa,” alisema.

Alisema kwa upande wa kusini, daraja hilo litaungana na Barabara ya Mandela kuelekea Tazara wakati upande mwingine utaungana na Barabara ya Kurasini kuelekea Kamata na zote kwa pamoja zitafanyiwa matengenezo ili kupunguza msongamano wa magari.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhan Dau alisema tathmini ya awali ya ujenzi wa daraja hilo ilianza mwaka 1977... “Ilipofika mwaka 1991, Serikali iliendelea na upembuzi yakinifu chini ya Kampuni ya Gauff ya Ujerumani ambayo ilionyesha gharama za ujenzi huo kuwa ni zaidi ya Dola 47 milioni.”

“Kutokana na ukosefu wa fedha ujenzi huo ulishindikana. Mwaka 2002, NSSF walianza mazungumzo mapya na kufanya upembuzi yakinifu mwaka 2003 na ilipofika mwaka 2005, shirika hilo liliingia mkataba na kampuni ya Arab Consulting Engineers ya Misri kwa ajili ya upembuzi wa kina. Kampuni hiyo ilishauri kuwa mradi usingeweza kuwa na faida kibiashara mpaka Serikali itoe ruzuku.” 

Apiga vijembe
Akizungumza katika hafla ya kutiliana saini mkataba huo, Waziri Magufuli aliwapiga vijembe wanasiasa wanaomshambulia kwa uamuzi wake wa kuongeza bei ya Kivuko cha Kigamboni akisema: “Maendeleo ya nchi hayaangalii itikadi ya chama, iwe CCM, Chadema, CUF na vyama vingine.”



Alisema kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Serikali ili kuleta maendeleo.
Alisema mambo ya siasa yanachangia kuongeza chuki, migongano na vurugu za hapa na pale, hivyo akasisitiza umuhimu kwa Watanzania kuyaepuka.

Waziri huyo alisema mkakati wa Serikali ni kutekeleza ahadi ilizoahidi wakati wa uchaguzi na si kulumbana wala kugombana.Aliwataka Watanzania kutambua kuwa siasa ni mambo ya mpito, lakini mwisho wa siku wataalamu wataendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Ninawaomba wananchi waache mambo ya siasa ili kutoa nafasi kwa wataalamu kufanya kazi zao na si kuwaingilia kwa sababu siasa inapoteza muda na kurudisha nyuma maendeleo... jamii inapaswa kujifunza mambo hayo,” alisema Dk Magufuli.

No comments:

Post a Comment