Wednesday, January 11, 2012

Yamemkuta tena,Kafulila atiwa mbaroni Kigoma

Anthony Kayanda, Kigoma
POLISI mkoani Kigoma  wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha NCCR Mageuzi waliokuwa kwenye mkutano ambao ulipaswa kuhutubiwa na mbunge  Kigoma Kusini, David Kafulila.

Habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Kazuramimba ambako Kafulila alikuwa amejiandaa kufanya  mkutano wa hadhara na tayari alikuwa ameanza kuhutubia akiwa kwenye gari na madiwani wawili wa chama hicho cha upinzani.


Kafulila aliliambia gazeti hili jana kuwa polisi hao walizuia mkutano wake na kumkamata kwa mahojiano yaliyodumu kwa takriban dakika 30, kwa madai kwamba mkutano wake haukufuata taratibu za kuomba na kupata kibali.


Kafulila ambaye yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kichama, alisema alipofika kijijini hapo alipata taarifa kwamba polisi wa kituo kidogo kilichopo eneo hilo waliwazuia viongozi wa NCCR Mageuzi kufanya maandalizi ya mkutano huo.


Alisema baada ya kusikia uamuzi huo, alilazimisha wafanye mkutano kwa vile yeye ni mbunge halali wa jimbo hilo la Kigoma Kusini na anapaswa kuzungumza na wananchi kuelezea utendaji wake wa kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.


“Polisi wamenizuia kufanya mkutano wangu na wametumia nguvu kubwa kututawanya kwa madai kwamba wametumwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kigoma (OCD), Japhet Kibona eti sisi hatujatimiza masharti..., na pia hatujaomba kibali cha kufanya mkutano. Sasa mimi kama mbunge wa jimbo nazuiliwa kwa nini?," alihoji Kafulila na kuendelea:


"Inawezekana huyu OCD ananihujumu na tayari nimewaeleza wakuu wake wa kazi kuanzia IGP,  Said Mwema na Waziri wa Mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha ili wajue hujuma ninayofanyiwa na huyu OCD wa Kigoma,"alisisitiza Kafulila.
Kafulila ambaye hatma ya ubunge wake iko mikononi mwa Mahakama baada ya kuvuliwa uanachama wa NCCR-Mageuzi, alisema katika sakata hilo walikuwepo polisi watano waliovurumisha mabomu ya machozi.


Alisema yeye alikamatwa na kupelekwa kituo kidogo cha Polisi Kazuramimba kwa mahojiano yaliyodumu kwa zaidi ya nusu saa, kabla ya kuachiwa huru kwa sharti la kutoendelea na mkutano wa hadhara.


Alisema kuzuiwa mikutano yake kulianzia Kijiji cha Ilagala ambako hata hivyo anaeleza kuwa mkutano ulifanyika kwa busara za Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, ACP Frasser Kashai baada ya kuwa umezuiliwa na askari wa Kituo kidogo cha Polisi Ilagala. 


RPC Kigoma
RPC Kashai alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kilichotokea ni mbunge huyo kukaidi na kukiuka utaratibu wa kisheria katika kufanya mikutano yake ya hadhara, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa ya maandishi polisi ili waweze kuandaa ulinzi.

"Sheria inatamka wazi kwamba, lazima wanaofanya mkutano watoe taarifa polisi kupitia kwa OCD saa 24 kabla, ili na sisi tujipange kwa ajili ya kuweka usalama unakuwepo, sambamba na kujiridhisha kama hakuna mkutano mwingine unaofanyika katika eneo wanalokusudia kufanya mkutano wao," alisema Kamanda Kashai.

Hata hivyo, alikanusha kutokea vurugu zozote katika mkutano huo bali ni kitendo cha polisi kuwazuia wananchi wasihudhurie kutokana na utaratibu kukiukwa, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na Polisi.
"Kafulila anafanya mambo ya ajabu sana kwa sababu siamini kwamba, hajui sheria na utaratibu wa kufanya mikutano ya hadhara, yeye ana tabia ya kuleta barua siku hiyo hiyo ya mkutano, lakini sheria inaeleza bayana ni lazima taarifa iletwe saa 24 kabla," alisisitiza Kashai.

Alisema hadi jana hakuwa amepata  taarifa zozote za kuwepo kwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo, hali inayoashiria  kwamba hapakutokea vurugu zozote.

Kafulia livuliwa wadhifa wa ukatibu mwenezi wa NCCR Mageuzi, tukio lililofuatiwa na kuvuliwa uanachama katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyika Desemba 17, mwaka jana.


Mbunge huyo alikuwa akituhumiwa kuratibu mpango wa mapinduzi dhidi ya mwenyekiti James Mbatia, pia kukiuka taratibu na katiba ya chama kwa kuzungumza baadhi ya mambo nje ya vikao vya chama.


Uamuzi huo ulikuwa unampotezea ubunge wake lakini, alikimbilia mahakamani kufungua kesi ya msingi kupinga uamuzi huo huku pia akiomba pingamizi la mahakama dhidi ya uongozi wa NCCR-Mageuzi, kuuzuia usitekeleze kitu chochote hadi kesi hiyo ya msingi itakapomaliza.   

No comments:

Post a Comment