Wednesday, January 11, 2012

HATIMAYE DUDE AMSAKA NDIKUMANA





SAKATA la minong’ono na madai ya kuwa mtoto wa wanandoa, Irene Uwoya na Hamad Ndikumana ‘Kataut’, ni wa staa wa filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’,  limechukua sura mpya baada ya Dude kuibuka na kusema: “Namsaka Ndikumana.”


Akizungumza na Risasi Mchanganyiko katika mahojiano maalum wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam, Dude alisema anamtafuta Ndikumana usiku na mchana ili amweleze ukweli anaoujua tofauti na uvumi uliozagaa kuwa anahusika na mtoto wa Uwoya.
ANAMSAKA USIKU NA MCHANA
Alisema, kwa muda mrefu imekuwa ikienezwa kwamba mtoto wa wanandoa hao ni wake, jambo ambalo si la kweli kwa vile hajawahi kutoka na Uwoya hata siku moja.
“Uwoya ni msanii mwenzangu, kwa maneno mengine Ndiku ni shemeji yangu. Sijawahi kutembea naye (Uwoya) na siwezi kutoka na mke wa mtu.
“Haya mambo yanakuzwa, naishi kwa wasiwasi. Sina amani. Sijui Ndiku anafikiria nini kichwani mwake, ndiyo maana nimeona si vibaya nikamtafuta ili nizungumze naye kiume.
“Hili si jambo la kulikalia kimya. Kwa kweli linanisumbua sana akilini mwangu. Namsaka usiku na mchana. Nataka kuzungumza naye ili kuondoa utata.”

APATA KIGUGUMIZI
Hata hivyo, Dude alipotakiwa kueleza ukweli alionao ambao anataka kumweleza Ndiku, aligoma kueleza chochote kwa madai kuwa anachotaka kukisema kinamhusu Ndiku pekee.
“Siwezi kuzungumza chochote, hata nikisema haitasaidia kitu. Natakiwa kukutana na Ndiku mwenyewe. Yeye ndiye anayetakiwa kuambiwa na mimi. Si mtu mwingine yeyote.
“Kama nilivyokuambia awali, haya mambo yanakuzwa. Si ya kuyakalia kimya... naujua ukweli wa hili suala lakini natakiwa kuzungumza naye tu,” alisema Dude na kuongeza:
“Naamini hatakataa wito wangu... nakumbuka hata kwenye birthday ya Uwoya, nilimwita pembeni nikazungumza naye, ingawa sikuweza kuongea naye suala la mtoto kwa vile watu wengi walikuwa wakimvuta na kuongea naye.”
Akaongeza: “Nilimwambia nitamtafuta muda mwingine...naona ndiyo muda wa kuweka sawa kuhusu suala la mtoto ambalo linazua mjadala mkubwa nikitajwa kuhusika. Nitazungumza naye ndani ya siku mbili tatu hizi, mambo yatakuwa sawa.”



AGOMEA DNA
Katika hali ya kushangaza, pamoja na kwamba Dude alimhakikishia mwandishi wetu kuwa hahusiki kwa namna yoyote na mtoto wa wanandoa hao, lakini alipoulizwa kama atakuwa tayari kuchukuliwa kipimo cha vinasaba (DNA) na mtoto huyo, aligoma.
“Nini, DNA? Kwa nini nipime sasa wakati nimeshasema sihusiki? Kiukweli kuhusu hilo, hata nikiwekewa mtutu wa bunduki mbele yangu, sipimi,” alisema na kuongeza:
“Kupima maana yake ninaungana mkono na hao wanaosambaza hizi taarifa. Ninachojua mimi ni kuwa sijawahi kutembea na Uwoya, hiyo inatosha, kama hawaamini basi!”

MASTAA WANENA MAZITO
Wakati huohuo, BRIGHTON MASALU anaripoti jinsi mastaa wa filamu Bongo walivyotoa maneno mazito, katika mjadala usio rasmi juu ya mgawanyiko wa ndoa hiyo.
 Wakizungumza kwa staili ya kushambulia, mbele ya mwandishi wetu hivi karibuni, Sinza-Mori, Dar, mastaa hao, Vincent Kigosi ‘Ray’, Jacob Steven ‘JB’, Blandina Chagula ‘Johari’ na Steven Mangere ‘Nyerere’, walieleza mitazamo yao juu ya mtafaruku wa ndoa hiyo.

RAY
“Ndikumana ni mkimya lakini ana matatizo. Nilimwambia kabla kuwa anataka kukurupuka, baadhi ya wanawake si wa kuolewa, lakini hakusikia. Hata hivyo ana ukorofi wake (Ndiku), hapendi kusikiliza ushauri na kibaya zaidi ana wivu kupindukia.”

JB
“Nahisi Uwoya hampendi Ndikumana, kampotezea muda wake... huyo mwanamke atateseka sana. Na mimi nadhani kuna kitu ambacho sisi hatukijui, ipo siku kitajulikana lakini Uwoya ana makosa sana hasa aliposema hajawahi kumpenda mumewe. Hata kama ni mimi ningeumia.”

JOHARI
“Jamani nyie hamjui tu, anayoyaona Uwoya kwenye ndoa yake ni ya kutisha. Simtetei kwa kuwa ni rafiki yangu lakini najaribu kukumbuka aliyoniambia, kama ni kweli ni halali waachane kuepusha mengi. Ndikumana ana matatizo,” alisema bila kufafanua zaidi.

STEVE NYERERE
“Hivi mwanaume na akili zangu naweza kuoa mwanamke kama Uwoya? Si nitakuwa najichimbia kaburi langu mwenyewe? Nakumbuka siku moja Uwoya alipanda taxi, Ndikumana akawa anamzuia na baada ya kuondoka jamaa akaanza kulia,” alisema Steve Nyerere, ambapo Ray aliunga mkono kauli hiyo.

KALAMU YA MHARIRI
Ndoa ni muunganiko mtakatifu, pamoja na mzozo uliopo kati ya wanandoa hao, bado wanayo nafasi ya kukaa na kuyamaliza. Familia zao zikitumia nafasi yao vizuri, zinaweza kurejesha amani katika uhusiano wao.

No comments:

Post a Comment